Jeshi la Magereza lawasilisha taarifa za utekelezaji wa sheria ya Bodi za Parole kwa Agustino Lyatonga Mrema
Jeshi la Magereza nchini limekabidhi rasmi ripoti ya taarifa ya utekelezaji wa sheria ya bodi za Parole kwa Mwenyekiti wa bodi hiyo Taifa, Agustino Lyatonga Mrema ikihusisha uelewa na elimu juu ya mambo ya Parole.
Tukio hilo limefanyika mapema leo Septemba 6.2016 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo la Magereza Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Magereza ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Parole ya Taifa, Bwana John Casmir Minja aliwasilisha taarifa hiyo ambapo imebeba maudhui mbalimbali ikiwemo ya kujenga uelewa juu ya Parole kama sheria ya Parole na utekelezaji wake.
Hii ni pamoja na sifa za mfungwa wa Parole, muundo wa bodi ya taifa, kitaifa na bodi za ngazi ya mikoa. Utendaji wa kazi kwa bodi ya Taifa ya Parole na bodi za ngazi ya mikoa, mafanikio na changamoto ya bodi ya Parole kitaifa na katika ngazi ya mikoa.
“Nimeipokea taarifa yenu ya bodi ya Parole na mimi kama Mwenyekiti nitahakikisha panapo tatizo tunasaidiana. Na yale magumu kama tatizo la bajeti ya kuhakikisha Parole haikwami nitaiwasilisha mimi mwenyewe kwa Rais John Pombe Magufuli” amesema Mrema
Ameongeza kuwa: “Kama hakuna pesa tusitegemee miujiza kwa Parole kufanya kazi na hii ni kutokana na ufinyu wa bajeti. Lakini labda tu nieleweshe jamii kwamba nilipopewa kazi ya kuwa mwenyekiti wa bodi ya Parole ya Taifa watu walidhani kwamba nakwenda magereza halafu nifungue milango wafungwa watoke, Hapana si hivyo, hili jambo lina mchakato mkubwa na mrefu,” ameongeza Mrema
Aidha Dkt.Mrema ametoa rai kwa jamii kuepuka kufanya uhalifu na kusema kuwa Magereza si mahala pazuri kupeleka nguvu kazi ya Taifa
“Magereza si mahala pazuri kwakweli, ni sehemu mbaya amabyo mtu anatakiwa aende kwa bahati mbaya tu.la muhimu ni kuwa jamii iepukane na vitendo vya uhalifu kwani nguvu kazi ya Taifa inapotelea jela”
Katika suala lingine Dkt. Mrema amewataka wananchi hususani vijana kuachana na makundi yanayohamasisha migomo na maandamano yasiyo na tija kwenye Taifa
“Labda tu niseme kwamba kufanya maandamano ya Lazima ni uhaini. Wenyewe wanayaita maandamano yasiyo na kikomo, hayo ni uhaini niwaombe wananchi wote hususani vijana waache kutumika na makundi yanayohamasisha maandamano dhidi ya serikali na uongozi uliopo madarakani” amesema Mrema
..hivi sasa mitaani kwetu kuna wafungwa watarajiwa wengi na mahabusu watarajiwa wengi hvyo wazazi wakanyeni vijana wenu wasijihusishe na vitendo vya uhalifu vitakavyowapelekea kwenda gerezani” amemalizia Dkt. Mrema.
Afisa wa Jeshi la Magereza (aliyesimama kushoto) akisoma taarifa ya utekelezaji wa sheria ya bodi ya parole kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Dkt. Augustine Mrema (wa kwanza kulia) wakati Mwenyekiti wa Bodi alipomtembelea Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini ambaye pia ni Katibu wa bodi ya Parole John Casmir Minja (katikati) mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini ambaye pia ni Katibu wa bodi ya Parole John Casmir Minja akimkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Dkt. Augustine Mrema wakati alipomtembelea ofini kwake ili kujua matatizo mbalimbali yanayoikabili bodi hiyo mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Dkt. Augustine Mrema akiagana na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini ambaye pia ni Katibu wa bodi ya Parole John Casmir Minja wakati Dkt. Mrema alipomtembelea ofisini kwake mapema hii leo jijini Dar es Salaam. Picha na Eliphace Marwa
No comments