Wakazi wa Magome Kota kuishi miaka 5 kwenye nyumba za kupanga bila kulipa kodi .....Wanaodaiwa na NHC Wapewa Siku 7
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota kukaa kwenye nyumba za Serikali miaka mitano bure na baadaye kuzinunua kwa bei nafuu.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akiwahutubia wakazi wa Magomeni na kuagiza ujenzi wa nyumba hizo kuanza ndani ya miezi miwili.
“Nasema wakandarasi ndani ya miezi miwili waanze kujenga nyumba 644 kwa ajili ya wazee ambao wameteseka sana baada ya nyumba zao kuvunjwa, nitatoa fedha Serikalini mwezi huu kwa ajili ya kuanza kwa shughuli hiyo” alisema Dkt. Magufuli.
Ameongeza kusema kuwa ujenzi huu anataka ukamilike ndani ya mwaka mmoja au miezi sita kama ulivyokuwa kwa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema atafurahi kukabidhi hati kwa wakazi wa Magomeni Kota pindi nyumba hizo zitakapokuwa zimekamilika.
“Namuomba Mwenyezi Mungu anipe uzima ili nyumba hizo zikiwa tayari hati nizikabidhi mwenyewe,”alisema Magufuli.
Rais Magufuli ameonyesha kukerwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu kuwanyima haki wanyonge. Amesema vitendo hivyo vya unyanyasaji viishe mara moja na watanzania wakae kwenye nchi yao kwa amani.
Aidha, Rais Magufuli amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kukusanya madeni yote ya kodi kwa wanaodaiwa na shirika hilo bila kujali chama, serikali au mtu yeyote.
Ameagiza kuwa wanaodaiwa inabidi walipe deni lao ndani ya siku 7 (saba) vinginevyo waondolewe kwenye nyumba hizo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali wanyonge hasa kwa kutatua mgogoro wa makazi kwa wakazi wa Magomeni Kota.
“Mheshimiwa Rais ninakushukuru kwa kuwajali wazee hawa wa Magomeni, nami nilitekeleza maagizo yako na kufuatilia mgogoro huu hadi kupata ufumbuzi”, alisema Lukuvi.
Lukuvi amesema kuwa mgogoro wa Magomeni ulivyokuwa mkubwa ulistahili nguvu ya Mhe. Rais Magufuli, lakini kwa migogoro mingine ambayo ni midogo, hiyo ameishughulikia na ataendelea kuishughulikia ili kero za wananchi kuhusu ardhi ziishe kama alivyoagizwa na Rais.
Nyumba zilizokuwa Magomeni Kota zilivunjwa mwaka 2009 na wananchi wakaahidiwa kujengewa nyumba ambazo wangeuziwa kwa bei nafuu. Lakini kwa takribani miaka mitano nyumba hizo hazikujengwa hali ambayo iliwafanya wakazi hao waishi maisha ya kuangaika.
Hivi karibuni Mhe. Rais John Pombe Magufuli alifuta hati zote za umiliki eneo la Magomeni Kota na kuondoa usimamizi wa Nyumba TAMISEMI na kuupeleka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuanza kusimamia ujenzi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipeana mikono na Mwenyekiti wa waliokuwa wakaazi wa nyumba za Magomeni Kota Bw. George Abdi wakati alipotembelea na kuongea na wakaazi hao wa Magomeni Kota jijini Dar es salaam leo Septemba 6, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimfariji Bi. Mwajuma Sama kwa taabu walizopata yeye kiongozi na wakaazi wenzie wa Magomeni Kota jijini Dar es salaam leo Septemba 6, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimshukuru wakili Twaha Taslima wa Law Chambers kwa kusimamia vyema maswala ya mgogoro wa eneo iliyokuwa Magomeni Kota jijini Dar es salaam leo Septemba 6, 2016. PICHA NA IKULU
No comments