‘Acheni kuweka vyakula vya moto kwenye plastiki ili Msipate Magonjwa’
SERIKALI imewataka Watanzania kuacha kuweka vyakula vya moto katika mifuko ya plasiti kutokana na uwepo wa uwezekano wa kupata magonjwa mbalimbali.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Stephen Masele wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mkiwa Adam Kimwanga (CUF).
Katika swali lake Kimwanga alitaka kauli ya Serikali kuhusu madhara ya uwekaji wa chakula cha moto katika mifuko ya plastiki na kauli Serikali kuhusu uchafuzi wa mazingira kutokana na kuzagaa kwa mifuko hiyo.
Masele alisema kuweka chakula cha moto katika mifuko ya plastiki kunakuwepo uwezekano wa kemikali zilizotumika kutengeneza mifuko hiyo kuingia kwenye chakula na kukifanya kuwa sumu.
“Sumu hii yaweza kusababisha saratani, kuharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi hususan kwa watoto ambao bado kuzaliwa, mabadiliko ya kijenetiki, matatizo ya kuona, uyeyushaji wa chakula tumboni kuwa taabu au kutokamilika na ini kushindwa kufanya kazi,” alisema.
Alisema madhara mengine ni pamoja na kuharibika kwa mfumo wa utendaji wa figo na magonjwa yanayohusiana na mfumo wa kupumulia.
“Ninawashauri wananchi wasitumie mifuko ya plastiki na vifungushio vyake kuwekea na kuhifadhia chakula kutokana na madhara yanayoweza kutokea,” alisema.
Aliwataka badala ya kutumia mifuko hiyo watumie vifungashio vya glasi, chuma isiyoshika kutu na vyombo vingine vya asili.
Alisema pia Serikali inatambua uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki na inachukua hatua mbalimbali ikiwemo kupiga marufuku matumizi ya mifuko laini yenye unene wa chini ya maikroni 30 na kuhamasisha matumizi ya mifuko mbadala.
Alisema pia Serikali inafanya ukaguzi kwa makampuni, maduka na viwanda vinavyozalisha na kusambaza mifuko ya plastiki nchini ili kujiridhisha kama vinazingatia sheria.
No comments