ACT Wazalendo wawapiga msasa wanachama wao
CHAMA cha ACT Wazalendo Mkoa wa Pwani kimeanza kuwapiga msasa viongozi wake wa ngazi ya kata na vijiji kama sehemu ya kuwaandaa kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Mafunzo hayo yameanza kutolewa juzi katika Wilaya ya Kibaha Mjini kwa kuwahusisha wenyeviti, makatibu, watunza hazina, wajumbe wa vikao mbalimbali na wanachama wengine.
Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Pwani, Mrisho Halphan, alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kutaka kila kiongozi atambue majukumu yake kulingana na eneo analofanyia kazi ili kukifanya chama kiwe imara.
“Chama chetu ni kipya, kwa hiyo, mafunzo hayo yatasaidia kuwapa washiriki uelewa mpana juu ya masuala ya kisiasa kabla uchaguzi wenyewe haujafika.
“Lengo letu tunataka kila kiongozi wetu aweze kutimiza majukumu yake bila kumuingilia mwenzake, kwani wakati wa mafunzo washiriki wanapewa sera na mikakati ya ACT katika kupambana na mafisadi,” alisema Halphan.
Pamoja na mafunzo hayo kuanzia wilayani Kibaha Mjini, Halphan alisema yatatolewa mkoa mzima wa Pwani kupitia Wilaya za Kisarawe, Bagamoyo, Mafia, Mkuranga, Rufiji na Kibaha Vijijini.
Akizungumzia uchaguzi mkuu, Halphan alisema chama chake kipo tayari kusimamisha wagombea kila ngazi, ikiwemo urais, ubunge na udiwani, kwa kuwa wamejipanga vizuri na wagombea wa nafasi hizo wanao.
Pia, aliwataka wananchi wasisikilize propaganda za watu wanaotaka kukiharibu chama hicho, kwa kuwa wanaamini kitakuja kuwa tishio kisiasa kwa siku zijazo.
No comments