Breaking News

VITA: CCM Waapa Kumng'oa Mchungaji Msigwa Jimbo la Iringa......CHADEMA Wajibu Mapigo, Waapa Kushinda Kata Zote 18 za Iringa



CHAMA cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Iringa Mjini, vimeingia katika tambo za kisiasa, kila kimoja kikijigamba kuibuka na ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
 
Pamoja na majigambo hayo, vyama hivyo vimewashambulia watendaji wa Halmashauri ya manispaa ya Iringa vikisema mbinu zao za kuwakosesha ushindi hazitafanikiwa.
 
Wakati CCM kupitia Katibu wake wa mkoa, Hassan Mtenga kimesema kuna wakuu wa Idara zaidi ya watano kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wengine wanakihujumu chama hicho, Chadema kupitia Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa imemrushia kombora Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Ahamed Sawa kikisema ameletwa mjini Iringa kwa lengo la kudhibiti ushindi wa Chadema.
 
“Tunazo taarifa, taarifa za uhakika kwamba, mkurugenzi huyo mpya ameletwa mjini Iringa kwa lengo la kudhibiti ushindi wa Chadema; mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na CCM wanazuia baadhi ya wapiga kura kujiandikisha katika maeneo wanayofanyia shughuli zao,” alisema Mchungaji Msigwa.

Naye Mtenga alisema; “Tunazo taarifa, taarifa za uhakika kabisa juu ya uwepo wa baadhi ya wakuu wa idara na watumishi wengine wa halmashauri ya manispaa ya Iringa kukihujumu chama chetu CCM,” alisema.
 
Alisema wanachosahau watumishi hao ambao hata hivyo hakuwataja majina ni kwamba hawajui mishahara wanayolipwa inatokana na juhudi za serikali ya CCM lakini ndio hao hao wanaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa na ufisadi unaoichafua CCM.
 
Akizungumza na wanahabari jana, Mtenga alisema Msigwa yuko bungeni Dodoma ili akawaage wabunge wenzake maana hatarudi katika bunge hilo baada ya Uchaguzi Mkuu.
 
Mtenga alisema katika uongozi wake wa miaka mitano, Mchungaji Msigwa ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi zikiwemo zile binafsi 84 alizozitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Mtenga alisema CCM yenye wanachama zaidi ya 70,000 katika jimbo la Iringa Mjini inatarajia kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kutumia mfumo wake imara wa chama katika ngazi zake zote.
 
“Tunayajua makosa tuliyofanya wakati wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa hadi Ukawa wakapata viti vya mitaa 65 huku chama chetu CCM kikipata 126; niwahakikishie hatutarudia kosa hilo na tunashukuru uchaguzi huo uliofanyika mwaka jana,” alisema.
 
Naye Mchungaji Msigwa aliita wanahabari kuzungumzia kazi ambayo yeye na wabunge wengine sita wa chama hicho wanaendelea kuifanya mkoani Iringa.
 
“Kama mnaangalia Bunge, tumebakiza wabunge watano tu bungeni kwa ajili ya kuwasilisha taarifa mbalimbali za upinzani. wengine wote tumetawanyika mikoani kwa ajili ya kuhamasisha watanzania kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema.
 
Msigwa alisema wanahamasisha watanzania wote wenye sifa wajiandikishe katika daftari hilo ili zoezi la kuomba kura litakapowadia kuwepo na kundi kubwa litakalotumia demokrasia kuchagua viongozi wanaowataka.

“Tunaingia katika Uchaguzi huo tukiwa na uhakika wa kuunda halmashauri katika baraza la madiwani la manispaa ya Iringa lakini kwa upande wa mbunge tuna hakika ya kupata kura zaidi ya 80,000,” alisema na
 
Huku wakiwa na imani ya kushinda ubunge na viti vingi vya udiwani vitakavyowawezesha kuunda halmashauri, Mchungaji Msigwa alisema pamoja na kuelekeza nguvu za kutosha katika kata zote, lakini za ziada zitapelekwa katika Kata ya Mlandege inayoongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi na ile ya Ilala inayoongozwa na Naibu Meya, Gervas Ndaki.
 
Jimbo la Iringa lina Kata 18, Chadema inadai kuwa ina uhakika wa kushinda Kata kati ya 14-10 ambazo zitawawezesha kuunda Halmashauri.

Aidha Mchungaji Msigwa alikanusha kutoa ahadi 84 wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010.

No comments