Wahamiaji haramu 250 wasambazwa magereza mbalimbali ya Tanzania
JUMLA ya wahamiaji haramu 250 kutoka nchini Ethiopia wapo katika magereza mbalimbali nchini.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima wakati akijibu swali la Mbunge wa Koani, Amina Andrew Clement.
Katika swali lake Mbunge huyo alitaka kujua idadi ya wahamiaji haramu kutoka Ethiopia walioko katika magereza nchini na hatua zinazochukuliwa dhidi yao wakishamaliza vifungo vyao.
Silima alisema katika Mkoa wa Kilimanjaro wapo wahamiaji 68, Lindi 34, Tanga 70, Mbeya 22, Morogoro 39, Mwanza 1, Pwani 4 na Mara 12.
“Hatua zinachukuliwa na Serikali kudhibiti wahamiaji haramu ikiwemo kuimarisha udhibiti, kuwashitaki na kuwarejesha makwao. Hatua zinazochukuliwa na Serikali baada ya wahamiaji haramu kumaliza vifungo au adhabu zao walizopewa na mahakama ni kuwaondosha nchini,” alisema.
Alisema urejeshaji wa wahamiaji haramu kutoka Ethiopia hufanyika kwa kutumia usafiri wa ndege kwa kuwa wameacha kutumia usafiri wa barabara kutokana na hofu ya kiusalama inayosababishwa na vitendo vya kigaidi.
Alisema hadi sasa jumla ya wahamiaji haramu 96 wamemaliza vifungo vyao kati yao wanaotoka Ethiopia wapo 91 na kwamba wanasubiri usafiri ili warejeshwe makwao.
No comments