Watu 15 Wauawa Kwa Mapanga Geita
WATU 15 wameuawa kwa kukatwa mapanga katika matukio tofauti mkoani Geita kwa imani za ushirikina.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema matukio hayo ya mauaji yametokea katika miezi mine kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu.
Konyo alisema mauaji hayo yametokana na imani potofu za ushirikina na wahusika wakubwa wa matukio hayo ni waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi.
“Kwa mwaka huu mpaka hivi sasa tulikumbwa na matukio 15 ya mauji yaliyotokana na imani za ushirikina ambako katika wilaya tano kulikuwa na wastani wa watu watatu ambao waliuawa, lakini tunashukuru matukio haya tumepungua kwa sababu ya operesheni ya kuwasaka waganga,” alisema Konyo.
Wakati huohuo, Kamanda Konyo amethibitisha kuwa mtu mmoja, Lyoba Juma (23), mkazi wa Kijiji cha Milwa Butiama amefariki dunia kwa kugongwa na gari ya Land Cruiser mali ya Mgodi wa GGM iliyokuwa likiendeshwa na Yusuph Hashibeli.
Alisema tukio hilo lilitokea ndani ya mgodi wa dhahabu wa GGM eneo la WD1 wakati Juma na vijana wenzake walipokwenda kupora mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu.
Kamanda alisema walinzi waliokuwa katika doria waliwafukuza na yeye aliteleza katika kifusi na kubiringika mpaka barabarani ndipo tairi za nyuma ya gari hiyo ilipomkanyaga kichwani.
No comments