Askari Azua Taharuki Akimsaka Mahabusu
TAHARUKI imeibuka katika majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa na kusababisha shughuli za mahakamani hapo, zikiwemo za kusikilizwa mashauri mbalimbali kusimama kwa muda wa takribani dakika 20.
Mtafaruku huo ulitokea baada ya askari kupiga risasi hewani mahakamani hapo wakati wakimsaka mahabusu aliyedaiwa kutoroka katika chumba cha mahabusu mahakamani hapo na kujificha darini.
Mwandishi wetu alishuhudia askari polisi wakiwa na bunduki mikononi wakihaha kumsaka mahabusu huyo ambaye alidaiwa kutoroka kupitia upenyo uliopo katika chumba cha mahabusi mahakamani hapo.
Mkasa huo ulianzia saa 5 asubuhi na kudumu kwa dakika 20. Hata hivyo, mahabusu huyo hakuweza kuonekana licha ya jitihada za baadhi ya polisi kupanda darini kupitia chumba cha mahakama namba mbili bila ya mafanikio.
Hekaheka za kumsaka mahabusu huyo zilianza pale baadhi ya watumishi wa mahakamani hapo na mahakimu kudai kusikia vishindo kwenye dari ambapo mara moja mahabusu waliokuwa kwenye chumba mahakamani hapo walihesabiwa.
Katika chumba hicho walitakiwa wawe mahabusu 10 lakini walipohesabiwa kwa mara ya kwanza ilibainika kuwa alikuwa amekosekana mmoja ndipo msako mkali ulipoanza huku askari wakihaha kumsaka darini.
Hata hivyo walipohesabiwa mara ya pili ilibainika kuwa hesabu yao ilikuwa imetimu kwamba walikuwa 10 lakini haikubainika nani miongoni mwao alikuwa ametoroka. Hata mahabusu wenyewe hawakuwa tayari kumtaja.
Habari za kuaminika kutoka mahakamani hapo zinaeleza kuwa baada ya watumishi wa mahakama hiyo wakiwemo askari polisi na mahakama kusikia vishindo vya miguu darini waliamini ilikuwa ni ya mahabusu anayedaiwa kutoroka katika mazingira ya kutatanisha siku tatu zilizopita.
No comments