SOMA:>> Diwani NCCR-Mageuzi afukuzwa Uanachama
CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimemfukuza uanachama Diwani wake wa Kata ya Kasulu Mjini, Isack Rashid kikimtuhumu kutoa siri za chama na kuzusha migogoro kati yake na viongozi wenzake.
Akitoa taarifa kwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, William Rutuli alisema kuwa halmashauri imepokea barua kutoka chama hicho juu ya uamuzi huo.
Rutuli alisema kutokana na barua hiyo, diwani huyo anakosa sifa za kuendelea kuwa mjumbe wa baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kasulu na hivyo kata hiyo kwa sasa kuwa wazi.
Mwenyekiti huyo alitumia nafasi hiyo kumshukuru diwani huyo (hakuwepo kwenye kikao) kwa kutumia muda wake wa karibu miaka minne na miezi kadhaa katika kusimamia maendeleo kwa wananchi wa kata ya Kasulu mjini na halmshauri hiyo kwa Jumla.
Akizungumza na mwandishi wetu, Diwani Rashid alikiri kupokea barua ya kuvuliwa uanachama kutoka kwenye chama chake hivyo kupoteza nafasi yake ya udiwani katika kata ya Kasulu mjini, ikiwa ni tuhuma tatu ambazo zimesababishwa kuvuliwa uanachama.
Hata hivyo, Rashidi alisema mchakato mzima wa kumvua uanachama, haukuwa halali kwani kikao maalumu cha Halmashauri kuu Zanzibar hakina mamlaka ya kumvua uanachama, kwani kinafanya kazi zake upande wa visiwani pekee.
Alisema kutokana na hali hiyo, amepinga kuvuliwa uanachama na kwamba ameanza kufanya mchakato wa kupinga kisheria kuvuliwa uanachama kwa kufuata taratibu na katiba ya chama hicho.
Kwa muda mrefu diwani huyo amekuwa kwenye mgogoro na Mbunge wa Kasulu mjini, Moses Machali, hali iliyosababisha kuwa na mashitaka katika ngazi mbalimbali za uongozi za chama hicho, kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuvuruga chama mkoani Kigoma.
No comments