Breaking News

Urais 2015: Pinda Asema Atafurahi CCM Wakimteua Profesa Mwandosa Kugombea Urais Iwapo Jina lake(Pinda) Litakatwa



WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye amechukua fomu za kuomba kuwania urais kupitia CCM, amesema atakuwa tayari kumuunga mgombea yeyote atakayepitishwa na chama chake. Alisema akikosa yeye  atafurahi akiteuliwa Profesa Mark Mwandosya.

Akitoa salamu  kwa wanachama wa chama hicho waliofika kumdhamini katika Wilaya za Mbozi, Mbeya  vijijini na Mbeya Mjini ambapo zaidi ya wanachama 6,000 walimdhamini, wakati wanaotakiwa ni 30.

Akisalimia wananchi wa Mbozi akitokea Rukwa, alisema katika Kanda ya Nyanda  za Juu Kusini, wamepata  heshima ya kuwa na wagombea wawili ikiwa ni yeye  na Profesa Mwandosya, hivyo  akishinda yeye itakuwa ni mipango  ya Mungu na akishinda  Mwandosya  pia  atafurahi kwa kuwa itakuwa ni heshima kwa wananchi wa kanda hiyo.

Alisema Chama hicho ili kishinde kinahitaji upendo na mshikamano. Alisisitiza kuwa  hakuna  maana ya kushambuliana na  kuchafuana  kutokana na kuwa waliochukua  fomu wote ni wana-CCM  na hadi sasa hakuna mwenye uhakika  wa kushinda  kutokana na siri hiyo   Mungu pekee  kuijua.

"Anayejua hadi sasa  kuwa  Rais wa Tano  wa Tanzania  ni nani  ni Mungu pekee na hivyo  hakuna  maana  ya kushambuliana kwani tunaweza kufika  mwisho wa safari wakiwa vipande vipande na hivyo kuzalisha  makundi makubwa  ndani ya chama ambayo yatakipa shida chama kupata ushindi wa kishindo," alisema.

Alitaka wagombea kuacha kujiaminisha ushindi kwa jambo ambalo alisema haliwezekani kwa wao kuwa na uhakika wa jambo hilo kutokana na ukweli kuwa anayejua mshindi ni Mungu  peke yake.

"Wako watu  hadi sasa  utawasikia wanasema kuwa lazima mimi  niwe  mimi,lazima  niwe  mimi  jambo  ambalo si la kweli kutokana na kuwa  anayejua  hayo ni Mungu peke  yake  na  hivyo wanachotakiwa  kujua  kwa sasa ni kuwa kazi yao ni kueleza mikakati yao badala  ya kujipa  uhakika wa kushinda," alisema.

No comments