Lupumba Aiyumbisha UKAWA
Wakati bado haijafahamika lini mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) atatangazwa rasmi, imefahamika kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba, amekuwa ndiyo kikwazo cha kutopatikana kwa mgombea huyo.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu kwa siku nne sasa umebaini kuwa hatua ya Profesa Lipumba kukwepa vikao vya Ukawa, ni mkakati mahsusi unaolenga kukwamisha mchakato wa kupatikana mgombea urais wa umoja huo.
Ukawa unaundwa na Cuf, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD.
Taarifa kutoka ndani ya vikao vya Ukawa vimeeleza kuwa kikao cha kwanza cha umoja huo, Profesa Lipumba aliulizwa kwanini anataka kugombea urais na kujibu kuwa anaamini kuwa yeye ndiye bora kuliko wengine.
Hata hivyo, alipoulizwa kama amejiandaa vipi kirasilimali iwapo atateuliwa kuwania nafasi hiyo kupitia Ukawa, hakuwa na majibu ya kujitosheleza na badala yake ilibainika kuwa Cuf imejiandaa zaidi Zanzibar kuliko Tanzania Bara.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Profesa Lipumba amekuwa aking’ang’ania agombee urais na hata mkutano wa mwisho wa Ukawa ambao hakuhudhuria, inadaiwa kwamba ni mkakati wa kushinikiza ateuliwe yeye kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Katika vikao vya Ukawa, hoja kubwa imekuwa ni suala la mgombea urais, nafasi ambayo inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye tayari ameshachukua fomu kupitia chama chake cha Cuf pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, anayeungwa mkono na vyama vyote vinne.
Profesa Lipumba ameshagombea urais mara nne bila mafanikio, wakati Dk. Slaa aligombea mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili, akiwa ameitikisa CCM iliyopoteza asilimia takriban 20 ya kura za mwaka 2005.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, akizungumza na waandishi wa habari Julai 14, mwaka huu, alisema umoja huo utamtangaza mgombea wao wa urais baada ya siku saba ambazo zinaisha wiki hii.
Alisema wamekubaliana kutangaza mgombea baada ya siku saba ili kutoa nafasi kwa viongozi walioshiriki majadaliano hayo kutoa taarifa kwa wanachama wa vyama vyao juu ya mambo waliokubaliana.
Aidha, Mbatia alikanusha uvumi kuwa kada wa CCM na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ana mpango wa kujiunga na umoja huo ili apewe nafasi ya kugombea urais baada ya kukosa nafasi hiyo kupitia chama chake.
Mbatia pia alikanusha uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna mvutano mkubwa ndani ya Ukawa katika suala la mgombea urais ambao umesababisha Cuf kutaka kujitoa.
“Hakuna ukweli katika hilo na hata leo (jana), nimeongea na Profesa Lipumba kumtaarifu hatua tulioyofikia, hivyo hakuna mpasuko wowote,” alisema Mbatia.
Kabla ya taarifa hiyo ya Mbatia,Ijumaa iliyopita Ukawa walitoa taarifa ya kwamba wangemtangaza mgombea wake ndani ya saa 24, ahadi ambayo haikutimizwa.
No comments