Breaking News

Damu Salama waeleza changamoto na kusisitiza Damu ni bure kwa mgonjwa nchini

Image result for Dk Avelina Mgasa
MENEJA wa Kanda ya Mashariki wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), Dk Avelina Mgasa amesema bado kuna changamoto kubwa ya ukiritimba katika utoaji wa damu kwenye hospitali mbalimbali nchini.
Aidha, alisema mahitaji ya damu salama kwa mwaka nchini ni takribani chupa 300,000 ambazo ni sawa na chupa 75,000 kwa robo mwaka, lakini hadi sasa makusanyo ya damu yanayofanywa na Mpango kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali yanakidhi asilimia 70 pekee.
Dk Mgasa aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu zoezi la uchangiaji damu salama lililoandaliwa na kampuni ya Indian Expat Group (IEG) linalotarajiwa kufanyika leo.
Alisema baadhi ya hospitali nchini zimekuwa zikifanya ukiritimba katika utoaji wa damu jambo linalosababisha wananchi kuwa na malalamiko juu ya hospitali hizo na vituo vya kukusanyia damu salama.
Hata hivyo, Dk Mgasa alisema mahitaji ya damu kwa kanda ya mashariki ni chupa za damu 68,869 kwa mwaka ambayo ni sawa na chupa 17,217 kwa robo mwaka.
Aidha alifafanua kuwa kumekuwa na ongezeko la makusanyo ya chupa za damu, kwani kwa takwimu za robo mwaka Januari hadi Machi mwaka huu jumla ya chupa 13,292 sawa na asilimia 77 zilikusanywa ikilinganishwa na zilizokusanywa kipindi cha Aprili na June ambazo ni 15,068 sawa na asilimia 87 ya mahitaji.
Dk Mgasa pia alipongeza uongozi wa kampuni hiyo kwa kujitolea kuchangia damu salama huku akiwaomba Watanzania wengine kujitokeza kwa wingi ili kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine.
Akizungumzia shughuli hiyo, mwenyekiti wa kampuni ya IEG, Dk Lion Kasarla alisema, uchangiaji damu huo utafanyika katika jengo la Quality Center lililopo Barabara ya Pugu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 10 jioni.

No comments