Kingunge Ngombale Mwiru Avunja Ukimya.......Amtaka Mkapa na Ali Hassan Mwinyi Wamshauri Rais Magufuli Afanye Mazungumzo na Chadema Kuhusu Oparesheni UKUTA
Aliyekuwa kada wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru  amewaomba  marais  wastaafu, Rais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kuzungumza na Rais  John Magufuli ili aitishe kikao kati ya Serikali na Chadema kwa ajili ya  kusitisha maandamano yaliyopangwa kufanyika Septemba Mosi.
Kingunge  ametoa kauli hii  leo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari  wakati akiongelea  mvutano kati ya Chadema na serikali unaoendelea kwa sasa.
Chadema  kimeingia kwenye mvutano mkubwa na serikali kutokana na dhamira yake ya  kufanya mikutano na maandamano nchi nzima chini ya mwavuli wa Umoja wa  Kupinga Udikteta (Ukuta).
Hivi  karibuni, Rais John Magufuli alisisitiza kutoruhusu maandamano na  mikutano ya kisiasa na kuagiza kuwa, wanaotaka kufanya mikutano wafanye  ndani ya mipaka ya majimbo yao na si vinginevyo jambo ambalo Chadema  wanapinga.
Hali  hiyo imeibua mtikisiko mkubwa nchini huku kada mbalimbali ikiwa ni  pamoja na viongozi wa dini, wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida  wakitaka kupatikana suluhu kabla ya Septemba Mosi, tarehe iliyopangwa  kuanza maandamano na mikutano hiyo.
Kwenye  mkutano wake na wanahabari Kingunge anawalaumu viongozi wastaafu  wakiwemo marais pamoja na mawaziri wakuu kwa kukaa kimwa wakati huu  ambao nchi inatikishwa huku Katiba ya Jamhuri ikisiginwa.
Miongoni  mwa viongozi wanaolalamikiwa kutosikika ama kuchukua hatua zozote ili  kuilinda Katiba ni pamoja na Marais Wastaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi,  Benjamin Mkapa na Aman Abeid Karume (Zanzibar).
Viongozi wengine waliotajwa ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Cleopa Msuya; Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.
“Mzee Mwinyi yupo kimya, Mkapa kimya, Warioba kimya, Cleopa Msuya kimya, Amani Karume kimya,” amesema Kingunge na kuongeza;
“Ukimya  huu unatokana na nini? Hawa wote waliwahi kula viapo vya utii kwa  Katiba. Mimi nahoji, wazee wenzangu vipi mnakuwa kimya? Nawaambia kuwa  mnachofanya si sawa.
“Naomba wazee wote tujitokeze kuhesabiwa katika hili la uvunjifu wa Katiba na sheria.”
Kingunge  ambaye alihamia Chadema akitokea CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka  jana kutokana na kutoridhishwa na namna mchakato wa kumpata mgombea  urais kutoka chama hicho amesema, Chadema inatumia haki yake ya  kikatiba.
“Naomba  Rais Magufuli, akubali kuitisha kikao na Chadema ambacho pia wazee  wastaafu watahudhuria, akifanya hivyo hata sisi wazee tutawageukia  Chadema na kuwambia wasitishe mpango wao wa maandamano,” amesema.
Amesema  kwamba, kibaya zaidi Jeshi la Polisi linaandaa bunduki kwa ajili ya  kupambana na raia ambao hawana kitu na kuwa, hali hiyo haipaswi  kuvumiliwa.
Mwanasiasa  huo amesema, Chadema wameamua kutetea haki yao ya kikatiba na kisheria  kwa kufanyaa maandamano kote nchini, na kina wafuasi wengi hivyo si  jambo la kubeza.
“Upande  wa pili, lipo Jeshi la Polisi na watawala ambao wanaahidi kuwakabili.  Kwa bahati mbaya polisi na watawala hawatetei Katiba wala Sheria,” amesema.
Amesema  kuwa, Tanzania kwa sasa inakabiliwa na ombwe la uongozi na kwamba, nchi  imekosa watawala wenye sifa thabiti ya kuongoza taifa.
“Kwa  hakika, tatizo kubwa la sasa la nchi yetu ni ombwe la kiuongozi,  kwasababu kama ni watawala tunao kweli kweli, lakini tunachokosa ni  watawala wenye maarifa ya kiuongozi.
“Inashangaza kuona wazee wastaafu kukaa kimya wakati nchi inakabiliwa na tatizo linaloweza kutuangamiza.
“Upande  mmoja unanoa mapanga, unaanda bunduki kwa ajili ya kuchinja na kuua na  upande wa pili wapo raia tu, tena wasio na silaha zozote.”
Kingunge anasema, wananchi ambao serikali na Jeshi la Polisi wanajiandaa kupambana nao, wanalilia Katiba na sheria zifuatwe.
“Laiti  kama Chadema wangekuwa hawatetei Katiba na sheria, kungekuwa na kila  sababu ya kuwashughulikia, lakini kwa kuwa wanatetea Katiba na sheria,  kuna umuhimu wa kuyapa uzito madai yao,” amesema Kingunge.
Mwanasiasa  huyo amesema kuwa, mvutano wa sasa sio wa Chadema na serikali isipokuwa  ni suala la wananchi wote wa wenye mapenzi mema na taifa lao.
“Hili ni suala la kila mtu anayependa utawala wa Katiba, Sheria na Utawala Bora,” amesema.
 

 
 
 
No comments