Waziri Mkuu: Watumishi Watakaokula Fedha Za Chf Wafukuzwe Kazi Na Na Wafikishwe Mahakamani
WAZIRI  MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani  kwa watumishi wote wa sekta ya afya watakaobainika kula fedha  zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Pia  amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Stephen pamoja na Mganga Mkuu  wa mkoa huo, Dk. John Gurisha kusimamia na kulinda fedha  za CHF  zinazochangwa na wananchi  na kuhakikisha zinatumika kama  zilivyokusudiwa.
Waziri  Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati  akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye  jimbo la Kwela, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga.
"Kitendo  cha kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa lengo la kupata huduma za  afya kinawafanya wakatetamaa ya kuendelea kuchangia mfuko huo. Kama wako  watumishi wenye tabia hizo waache mara moja," amesisitiza.
Mbali  na kutoa agizo hilo kwa uongozi wa mkoa wa Rukwa, pia Waziri Mkuu  amewataka wananchi kujiunga na CHF kwa sababu mfuko huo utawawezesha   kupata huduma za matibabu bure wao na familia zao katika kipindi cha  mwaka mzima.
Wakati  huo huo Waziri Mkuu amesema barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze ye  urefu wa kilometa 85  itajengwa kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika  kwa urahisi na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati.
“Mimi  nilidhani mlima wa Kitonga ndio mkali kuliko yote na eneo la Sekenke  ndio linatisha zaidi!. Kumbe barabara ya kuja huku Mtowisa ndiyo  inatisha zaidi kuliko zote. Lazima tuweke lami ili iendelee kupitika kwa  urahisi zaidi,” amesema.
Akizungumzia  ombi lililotolewa na mbunge wa jimbo la Kwela, Ignas Malocha la kutaka  tarafa hiyo ya Mtowisa kuwa wilaya au halmashauri, Waziri Mkuu amesema  analichukua na kwenda kulifanyia tathmini na majibu atayapata kupitia  uongozi wa mkoa.
Malocha  alisema jimbo la Kwela linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya  miundombinu ya barabara hali inayosababisha wananchi kushindwa  kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
Pia  aliomba ukanda huo wa bonde la mto Rukwa upandishwe hadhi na kuwa  wilaya au halmashauri ili kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.
Kwa  upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa  Rukwa, Mhandisi Masuka Mkina ameelezea mkakati wa kuboresha miundombinu  ya barabara mkoani hapa ikiwemo ya kutoka Ntendo hadi Muze wilayani  iliyopo wilayani Sumbawanga.
Mhandisi  Mkina amesema Serikali imetenga jumla ya sh. milioni 170 kwa ajili ya  kuweka zege kwa ajili ya kurahisisha upandaji wa mlima hasa kwenye eneo  la Kizungu katika barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 24, 2016.
 

 
 
 
No comments