Oktoba Mosi Yaanza Kugombaniwa.......Makonda Aitangaza Kuwa Siku Ya Kupanda Miti Huku Akiwataka JWTZ Washiriki Zoezi Hilo
Siku moja baada ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kuahirisha kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kupitia oparesheni walioipa jina la UKUTA ( Septemba Mosi) na kisha kuitaja Oktoba Mosi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda nayeye ameitaja siku hiyo kuwa siku maalum ya kupanda miti.
Na ili kufanikisha zoezi hilo, Jeshi la Wananchi (JWTZ) limeombwa kushiriki huku mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akizuia mikutano yoyote ambayo itaonekana haina tija.
Chadema ilikuwa imepanga kuzindua operesheni iliyoibatiza jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), kwa kufanya mikutano na maandamano kote nchini, lakini ikatangaza kuahirisha juzi ikieleza kuwa imezingatia ushauri kutoka kwa viongozi wa dini, taasisi na watu mashuhuri.
“Nimezungumza na watu wa hali ya hewa, wameniambia tukianza mapema miti hii haitakufa. Siku ya Oktoba Mosi kila mtu atakuwa na mti wake, tutawaarifu kupitia wakuu wa wilaya miti itapatikana wapi baada ya taratibu zake kukamilika,” alisema Makonda jana mbele ya Rais Magufuli kwenye mkutano wa 14 wa wahandisi kwenye ukumbi wa Mlimani City.
Makonda alisema siku hiyo vikosi vya ulinzi na usalama vitashiriki kupanda miti na kumuomba Rais amsaidie na amvumilie ili atende kazi yake ya kuhakikisha mkoa wa Dar es Salaam unakuwa na amani sambamba na kufanikisha kutekeleza mpango huo wa upandaji miti.
Aidha, makonda alipiga marufuku kufanyika kwa mikutano au maandamano yoyote isipokuwa mikutano itakayokuwa inajadili shughuli za maendeleo.
Aidha, makonda alipiga marufuku kufanyika kwa mikutano au maandamano yoyote isipokuwa mikutano itakayokuwa inajadili shughuli za maendeleo.
“Watakaopewa kibali ni wale wanaojadili maendeleo, lakini si wapigakelele. Mikutano kama hii (ya wahandisi) inayojadili masuala muhimu kabisa kwa maendeleo ya nchi, itaruhusiwa bila shaka yoyote.”
Makonda alisema kampeni hiyo itawahusisha pia wananchi, viongozi wa dini na kamati nzima ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dar es Salaam na kwamba jumla ya miti milioni 4 inatarajiwa kupandwa siku hiyo.
Alisema ameamua kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa sababu ni watiifu na wazalendo kwa Taifa wakati kada nyingine zimejielekeza kwenye siasa.
Hata hivyo, Rais hakuzungumzia maombi hayo zaidi ya kusema kuwa Makonda naye amekuwa mhandisi kutokana na kutoa maelekezo.
Kabla ya Makonda kutangaza Oktoba Mosi kuwa siku ya kupanda miti, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wamekutana na viongozi wa dini zaidi ya mara moja kwa ajili ya kupata maoni na ushauri kuhusu maandamano yao, ambayo Jeshi la Polisi liliyapiga marufuku kwa maelezo kuwa yalikuwa na viashiria vya kuvunja amani.
Baadaye JWTZ ilisema ingeadhimisha kuzaliwa kwa jeshi hilo kwa askari wake kufanya mazoezi na kuonyesha silaha zao za angani na nchi kavu, kufanya usafi mitaani na kujitolea damu, huku likibainisha kuwa linaamini hakungekuwa na maandamano yoyote kwa kuwa yameshazuiwa.
Katika kuadhimisha miaka 52 ya JWTZ jana, Makonda alishiriki kufanya usafi na askari hao katika kambi ya Lugalo iliyopo wilayani Kinondoni.
Makonda aliambatana na kamati ya amani ya viongozi wa dini wa Dar es Salaam, ikiongozwa na mwenyekiti wake Alhadi Mussa Salum.
Makonda aliitaja barabara ya Mwenge –Ubungo kuwa ni miongoni mwa barabara zitakazopandwa miti siku hiyo na watashirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
No comments