Wanafunzi 3918 wachaguliwa kujiunga kidato cha tano kwa awamu ya pili
Taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe ilisema kati ya wanafunzi hao wasichana ni 2,413 na wavulana 1,505.
“Kuchaguliwa kwa wanafunzi hao kumefuatia kuwapo kwa nafasi zilizoachwa wazi na wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni tangu kuchaguliwa kujiunga na kidato cha Tano katika awamu ya kwanza” alisema Mhandisi Iyombe.
Aidha Mhandisi Iyombe alibainisha kuwa kati ya wanafunzi 1,864 sawa na asilimia 47.58 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya Sayansi na Hisabati ambapo kati yao wasichana 1,099 na wavulana 765.
Mhandisi Iyombe aliongeza kuwa katika masomo ya Sanaa na Biashara wanafunzi takribani 2,054 (52.42%) wamechaguliwa kujiunga na masomo hayo, ambapo kati yao wasichana ni 1,314 na wavulana 740.
“Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili mwaka 2016 wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangwa kwa wakati. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya tangazo hili atakuwa amepoteza nafasi hii” alisema Mhandisi Iyombe.
Majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili mwaka 2016 inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI ambayo ni www.tamisemi.go.tz.
No comments