Aesh Atishia Kuzichapa Bungeni
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aesh Hillary (CCM), ameeleza kushangazwa na kitendo cha Serikali kutenga Sh bilioni 15 kati ya Sh bilioni 80 zilizoombwa na Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) na kwamba iwapo serikali itafunga mipaka ya nchi ili chakula kisiuzwe nje, watashikana mashati bungeni.
Akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma jana Ijumaa aprili 6, Aesh alisema fedha hizo zilizotengwa zinatosha kunua mahindi Wilaya ya Sumbawanga pekee.
“Kama mkishindwa kununua haya mahindi msifunge mipaka, mwaka jana mmefunga mkaja kufungua wakati muda umekwenda na kuweka masharti magumu, nawaambia safari hii mkishindwa kununua mkafunga mipaka tutashikana mashati humu ndani.
“Siyo kazi ya mkulima kuhakikisha nchi haina njaa ni kazi ya Serikali, nashangaa huku mnasema tu tumbaku na pamba, bila mahindi huyo mkulima hawezi kulima hayo mazao yake,” alisema Aesh.
Aeshi pia amezungumzia watumishi wenye elimu ya darasa la saba kufukuzwa kazi akisema mmoja wa Madereva waliofukuzwa kazi alimwendesha mpaka Waziri Mkuu Mstaafu (hakutaja jina la waziri huyo).
“Huyu dereva alikuwa amebakisha miaka mitano tu astaafu, sasa hivi mmemfukuza kazi hana cha kufanya, suala hili mliangalie upya,” alisema.
No comments