Profesa Jay akumbuka msoto wa Maisha....Asimulia Alivyokuwa Anakunywa Maji ya Chooni na Kupanda Malori
Nguli wa muziki wa Bongo Fleva ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mikumi, Joseph ‘Profesa Jay’ Haule, amekumbuka msoto aliokutana nao wakati anatafuta kutoka kimuziki miaka ya 1990 akiwa na Hard Blasters Crew (HBC).
Akifunguka kupitia The Playlist ya Times FM, rapa huyo mkongwe aliyechonga barabara kwa wasanii wengi wa rap nchini, amesema kuwa wakati wanaandaa albam zao na HBC, hawakuwa na kitu mfukoni kiasi cha kufikia hatua ya kunywa maji ya bomba lililokuwa chooni ili waendelee kufanya kazi yao studio.
“Nakumbuka wakati huo tunarekodi, unaenda kunywa maji chooni hivi… kwenye bomba liliko chooni unakula na mihogo yako ili uweze ku -buy time ya kuendelea kuwa studio siku nzima. Kwamba hakuna hata pesa ya kula chips mzee,” Profesa alifunguka.
Mkali huyo wa rap mwenye majina mengi ya kupewa kwa kuwa mbabe wa kurap, alieleza kuwa wakati wamepata nafasi ya kurekodi albam yao kama HBC, kuna wakati akiwa anafanya kazi Tanga, ilimlazimu kupanda malori ya mizigo usiku ili arejee kazini Jumapili usiku, kwani muda wa usiku aliokuwa akimaliza kurekodi jijini Dar es Salaam, magari ya abiria hayakuwepo.
Katika hatua nyingine, Profesa Jay alieleza tukio la kurekodi wimbo wake wa ‘Jina Langu’ katika studio za Bongo Records chini ya mtayarishaji nguli, P-Funk Majani. Alisema alimshangaza Majani kwani alikuwa akisikia mara kadhaa mdundo wa wimbo huo, ndipo alipomuomba mtayarishaji huyo aingize sauti.
Alisema baada ya kuwekewa mdundo, alipita na mashairi yote matatu bila kukwama, kitu ambacho kilimshangaza Majani pamoja na ukubwa wa mashairi yaliyowekwa ndani.
Profesa amewashauri wasanii wa Tanzania kuendelea kuandika vitu ambavyo vinagusa jamii na kuitangaza Tanzania kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.
Hivi karibuni, aliachia wimbo wake ‘Pagamisa’ akiwa na mtayarishaji wa muziki, Mr. T-Touch.
No comments