Spika Ndugai: Suala la Matibabu ya Tundu Lissu ni Jipya na Linahitaji Muda
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema utaratibu wa Bunge kugharamia matibabu ya Tundu Lissu unaendelea kufanyiwa kazi na ukikamilika utatolewa ufafanuzi.
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo jana Alhamisi Aprili 5, 2018 wakati akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Azam ikiwa ni siku moja kupita tangu aliporejea nchini akitokea India kwa matibabu.
Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7, 2017 na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi ambako alilazwa hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, anakoendelea na matibabu.
Tangu wakati huo, familia yake na viongozi wa Chadema wamekuwa wakililalamikia Bunge kutogharamia matibabu ya mbunge huyo huku Lissu naye mara kadhaa akizungumzia jambo hilo.
Lakini katika mahojiano hayo aliyofanya na mtangazaji wa televisheni hiyo, Charles Hilary, Ndugai amesema, “Lile tukio (la kushambuliwa Lissu) limekuwa ni jipya, linataka watu wengi waweze kuangalia jinsi ya kufanya. Kwa kifupi kila anayekwenda kutibiwa nje anakuwa na barua ya Wizara ya Afya au kibali kutoka Muhimbili, ndivyo sisi Watanzania tunafanya.”
“Hiyo ni kwa mbunge na asiye mbunge, hata mwananchi wa kawaida utaratibu ndio huo. Sasa kwa mheshimiwa Lissu alivyotoka Dodoma kila mtu anafahamu alipewa rufaa Nairobi na ndio maana tunaona kwa wabunge wengine wote wanaotibiwa kwa utaratibu huu huwa hawachangiwi hata na Bunge lenyewe.”
Amefafanua zaidi kuwa, “lakini mheshimiwa Lissu pale pale tulichanga sisi wenyewe wabunge kama wabunge kwa sababu tulikuwa tunajua safari hii ina tatizo ndio maana ikabidi watu wachange kutoka mfukoni.”
Amesema ni sawa na mtu aliyekata rufaa yeye mwenyewe kwenda katika hospitali aliyochagua, “kwa maana ile hakuchagua yeye mheshimiwa Lissu lakini familia yake na chama chake na kadhalika, halijawahi kutokea jambo kama lile katika Bunge letu, lina upya wa aina yake.”
Amesema upya huo unahitaji ushirikiano mkubwa wa familia na Bunge kuweka utaratibu ambao hautakuwa kwa kwa Lissu pekee.
“Hata kesho na keshokutwa huo ndio utakuwa utaratibu utatumika siku zijazo, kwa hiyo bado linafanyiwa kazi siku ya siku litakuja kutolewa maelezo kama linawezekana au haliwezekani.”
Kuhusu wabunge kupewa ulinzi baada ya Lissu kushambuliwa, Spika Ndugai amesema Dodoma hali ya ulinzi ni kubwa.
“Dodoma ni salama na tumemwomba RPC wakati wa Bunge na wakati wote ulinzi uwepo na umeimarishwa na sidhani kama litatokea tena,” amesema.
No comments