MAAJABU YA DUNIA>> Fisi akwapua mtoto mgongoni kwa mamaye
Mtoto wa miezi mitatu, Ng’wanza Samweli, amekufa baada ya kukwapuliwa na fisi kutoka mgongoni mwa mama yake wakiwa njiani kwenda nyumbani kwao katika kijiji cha Ngugunu, wilayani Meatu mkoa wa Shinyanga.
Fisi huyo aliwashambulia mama na mtoto huyo katika kijiji hicho kilichoko kata ya Kisesa mkoani Shinyanga.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Gemini Mushy alisema tukio hilo ni la Mei 25 saa 1:30.
“Ilikuwa saa 1:30 usiku wa Mei 25, wakati mama wa Ng’waza alipostuka kuona mwanawe akitolewa mgongoni na fisi aliyetokomea naye kusikojulikana,” alisema.
Kamanda alisema polisi pamoja na wanakijiji waliendesha msako na kufanikiwa kupata baadhi ya viungo vya Ng’wanza, umbali wa meta tatu kutoka mahali alipokwapuliwa.
“ Fisi hatukuweza kumpata lakini tulifanikiwa kupata mabaki ya viungo vya mtoto huyo kikiwemo kichwa, kifua na tumbo. Miguu na mikono ilikuwa imekwisha tafunwa pamoja na mifupa,” alieleza.
Kamanda Mushy alisema kuwa, eneo walipovamiwa watu hao lina fisi wengi, ingawa si kawaida kuwavamia wapitanjia.
No comments