Lembeli: Sitagombea ubunge kupitia CCM>
Mbunge wa Kahama, James Lembeli ameiweka njiapanda CCM baada ya kutangaza kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho.
Uamuzi wa Lembeli umekuja wakati wanachama kutoka sehemu mbalimbali wakitangaza uamuzi wao wa kujiengua CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, hasa Chadema ambayo imesomba asilimia kubwa ya wahamaji hao.
Akizungumza jana baada ya kuzagaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa amekihama chama chake na kuhamia Chadema, Lembeli alisema taarifa hizo ni uvumi uliozagaa jimboni kwake, lakini hajajiunga na chama chochote.
“Ni uvumi tu na uvumi wenyewe umechangiwa na swali nililoulizwa leo na wananchi kwamba ‘mbona toka mchakato wa kuchukua fomu umeanza hatujakuona’ na mimi nikawajibu kuwa ‘sitachukua fomu’,” alisema.
Lembeli (pichani) alisema amechukua uamuzi huo kutokana na rafu inayoendelea jimboni humo na maneno ya baadhi ya wanachama, wakiwemo viongozi kuwa hatakiwi na vigogo ndani ya CCM.
Lembeli, mmoja wa wabunge waliokuwa mstari wa mbele wakati wa kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, alisema sababu za kutotakiwa huko zinatokana na dhana potofu ya baadhi ya viongozi kwamba michango yake ndani na nje ya Bunge inaivua nguo Serikali.
“Tangu mchakato wa uchukuaji wa fomu umeanza baadhi ya wanachama wengi tu wameitwa kwenye vikao visivyo halali karibu kata zote wakiwa na kadi zao na kuorodheshwa na kupewa maagizo ya kunikataa kwenye kura ya maoni na wengine wanapewa Sh5,000,” alisema
Lembeli alidai kuwa mbaya zaidi ni kwamba zipo kadi mpya za CCM zinazotolewa kiholela bila kufuata utaratibu na licha ya kulalamikia hali hiyo hakuna hatua zilizochukuliwa.
Alisema kutokana na yote hayo, aliwahi kusema kwenye mkutano wa hadhara kuwa kuna njama hizo, lakini badala ya CCM kufanyia kazi madai hayo, wakamuita mbele ya Kamati ya Maadili.
“Kwenye kamati ya maadili nilituhumiwa kuwa nakidhalilisha chama na kutakiwa niwataje nani walioniambia sitakiwi. Niliwajibu, tena kwa maandishi na kuwapa orodha, lakini mpaka leo kimya ina maana mimi bado ni mtuhumiwa,” alidai.
“Mimi siyo mtoto mdogo. Naelewa nini kinaendelea na ndiyo maana nimesema sitachukua fomu ya kugombea ubunge kwa mazingira haya. Bado sijatangaza kuhama CCM”.
Wakati Lembeli akisisitiza suala la kuhama kwake ni fununu tu, habari nyingine zilidai huenda akagombea ubunge kwa tiketi ya Chadema kutokana na kutokubaliana na mchakato huo anaodai ni batili.
Lembeli anaonekana kuwa mwiba ndani ya Serikali ya CCM baada ya kuiongoza Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ya Bunge katika uchunguzi wa uendeshaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili na kuibuka na taarifa iliyoonyesha kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Mawaziri hao ni Balozi Hamis Kagasheki, Dk. David Mathayo, Dk. Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na Ezekiel Maige.
Lembeli pia nusura ajikute nje ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2010 wakati alipopigiwa simu na katibu mkuu wa CCM wa wakati huo, akiambiwa achukue fomu za kuwania ubunge wa jimbo jipya la Ushetu.
Wakati huo, Lembeli alidokezwa siku ya mwisho na ofisa mmoja wa Tume ya Uchaguzi kuwa hakukuwapo na jimbo hilo na kulazimika kufanya jitihada katika muda mfupi kuchukua fomu kwenye Jimbo la Kahama na kufanikiwa kushinda kiti hicho.
Hivi karibuni, Lembeli alitofautiana na taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ya kuwasafisha mawaziri na katibu wa wizara waliowajibika kutokana na kashfa ya escrow na Operesheni Tokomeza.
Lembeli alisema kitendo cha kuwasafisha viongozi hao ni kuipeleka nchi gizani.
“Yuko hapa (waziri mkuu wa zamani, Edward)Lowassa. Japo mimi sipendi wizi na ufisadi, katika kashfa ya Richmond nilikuwa mmoja wa waliopiga kelele awajibike. Lakini wengine wamesafishwa, kwanini naye asisafishwe,” alisema baada ya taarifa hiyo ya Ikulu.
“Kama ni kusafishana tusafishwe wote, tuanze upya ndipo nchi hii itatawalika, vinginevyo huko mbele kuna giza nene.”
No comments