Mwinyi Avunja Ukimya Kilichotokea Dodoma...... Asema Haikuwa Kazi Rahisi Kumpata Mgombea wa Chama
Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa shughuli ya kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM haikuwa rahisi na akashukuru kwamba imemalizika kwa amani.
Mchakato huo ulihitimishwa Julai 12 mjini Dodoma wakati Mkutano Mkuu wa CCM ulipopitisha jina la Dk John Magufuli kugombea nafasi ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake mwishoni mwa mwaka.
Jumla ya makada 38 walijitokeza kuwania nafasi hiyo, na majina matano ndiyo yaliyopitishwa kwenda Halmashauri Kuu na baadaye matatu kwenda Mkutano Mkuu.
Mchakato wa urais ndani ya CCM ambao kwa kawaida hutawaliwa na msuguano kabla ya kumalizika kwa maridhiano, safari hii ulienda mbali zaidi baada ya wajumbe watatu wa Kamati Kuu kupinga nje ya kikao uamuzi wa chombo hicho na baadaye wajumbe wa Halmashauri Kuu kumwimbia mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete wimbo wa kuonyesha wana imani na Edward Lowassa baada ya jina la mbunge huyo wa Monduli kuenguliwa na Kamati Kuu.
Jana, akitoa hotuba fupi baada ya kumalizika kwa sala ya Eid el Fitr kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mwinyi alizungumza kwa mara ya kwanza hadharani kuhusu mchakato huo, akidokeza hali ilivyokuwa.
“Haikuwa kazi rahisi kwenye mchakato huu wa kumtafuta mgombea mmoja atakaye peperusha bendera ya CCM,” alisema Mwinyi lakini akawahi kuipoza kauli hiyo kwa kuelezea amani ilivyotawala mwishoni.
“Kama ni jahazi basi sasa tunashukuru limefika pwani salama.”
“Uchaguzi huu ni kwa ajili ya kuwapata viongozi wetu, tunataka viongozi bora wa kutuletea maendeleo, mapatano na wenye mahaba na wananchi.”
Akizungumza hadharani kwa mara ya kwanza baada ya mchakato huo wa kumtafuta mgombea wa urais kukamilika mjini Dodoma, Mzee Mwinyi alimshukuru Mungu kwa mchakato huo kuisha salama.
“Haikuwa kazi rahisi kwenye mchakato huu wa kumtafuta mgombea mmoja atakaye peperusha bendera ya CCM, kama ni jahazi basi sasa tunashukuru limefika pwani salama.
“Sasa, ninawaomba Watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi wa nchi tunaoufanyika kila baada ya miaka mitano,“ alisema Rais Mwinyi ambaye alikuwa mmoja ya wajumbe wa Baraza la Ushauri waliofanya kazi ya kutuliza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM hadi kuafikiana kuendelea na mchakato wa kumpata mgombea urais.
Aliwasisitizia Watanzania kuacha tabia ya kupenda mno na kuacha kubaguana, akisema hakuna aliye bora na kuwataka kuzidisha mapenzi miongoni mwao na kusherehekea vyema Sikukuu ya Eid el Fitr.
“Hakuna jambo lenye maana kama hili la kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kutufikisha salama siku kama hii ya leo (jana) ambayo tunasherekea Sikukuu ya Eid,” alisema Mwinyi.
“Hakuna jambo lenye maana kama hili la kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kutufikisha salama siku kama hii ya leo (jana) ambayo tunasherekea Sikukuu ya Eid,” alisema Mwinyi.
Awali Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum aliwasisitizia wananchi umuhimu wa kusherekea sikukuu hiyo katika hali ya amani na utulivu.
Pia, aliwashauri wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao sehemu zenye maadili ili washerehekee kama ambavyo Mwenyezi Mungu anapenda.
“Leo (jana) ni siku ya furaha, naomba tusherekee maeneo salama pia Waislamu msisahau kufunga sita kwani ina malipo makubwa,” alisema Alhad Salum.
Mkoani Geita ambako ilifanyika sala ya kitaifa ya Eid, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alihutubia Baraza la Eid na kusema kipindi hiki kinahitaji utulivu, kuelewa na kuheshimiana pamoja na kudumisha uhusiano ili Taifa lipate viongozi bora.
“Tuwe watulivu ili Tanzania ibaki kuwa nchi ya kukimbiliwa na isiwe nchi ya kukimbiwa... sisi tusiwe wakimbizi, tuwe watu wa kupendana, kuvumiliana na kuthaminiana. Tusifikie hatua ya kuchukiana, kuuana na kufanyiana ukatili,” alisema Dk Bilal.
Alisema amani inaweza kuvunjwa na mtu yoyote kwa namna yoyote ile, akaharibu mazuri na heshima ya Taifa na akawaomba wananchi na waumini wote wasifikie hatua hiyo akisema ndiyo wenye uwezo wa kuifanya nchi yao kuwa ya amani.
“Tuishi kwa kuheshimiana, kupendana na kuvumiliana tushikamane katika, hali iliyopo sasa kwa nchi yetu siyo nzuri. Si ajabu hivi sasa tunavyoongea kuna sehemu mabomu yametokea, si ajabu kuna watu wameuawa kikatili. Hii yote ni sababu watu sasa wanapoteza misingi ya kuheshimiana, upendo na kuvumiliana,” alisema Bilal kwenye Viwanja vya Karangara.
Awali Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania, Bakwata, Sheikh Suleiman Lolela alisema waumini na wananchi wote waitumie vyema nafasi ya Uchaguzi Mkuu kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaoendeleza amani.
Kisiwani Unguja, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein amewataka viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kijamii na madhehebu ya dini kulinda na kuheshimu msingi na malengo ya kuanzishwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akiuhutubia kwenye Baraza la Eid el Fitr lililofanyika Ukumbi wa Bwawani na kuhudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad jana, Dk Shein alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kufanya siasa kwa kuzingatia misingi ya Katiba na sheria kwa madhumuni ya kuendeleza na kulinda amani na umoja wa kitaifa kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
“Tunaweza kushindana bila ya kulaumiana, kukejeliana na tunaweza kushindana bila ya kudharauliana au kuhasimiana,” alisema Dk Shein kwenye shughuli hiyo iliyotaliwa na hali ya utulivu.
Alieleza kuwa vyama vya siasa vimeanzishwa na vipo kwa ajili ya kushindana kwa sera kwa madhumuni ya kuchochea maendeleo ya Zanzibar na siyo kugombanisha watu na kuvuruga misingi ya amani na umoja wa kitaifa.
Kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, sheikh wa mkoa, Ahmed Zuber aliwataka Watanzania kudumisha amani na umoja.
Zuber alisema dunia sasa imechafuka kutokana na uvunjifu wa amani unaochochewa na siasa chafu hivyo Watanzania bila kujali dini wala itikadi zao wanapaswa kuilinda amani iliyopo sasa.
“Tunahitaji utulivu. Nchi nyingi huharibikiwa kipindi kama hiki cha uchaguzi, amani hupotea kipindi hiki cha uchaguzi. Ndugu zangu Waislamu na msio Waislamu tukiichezea amani hii iliyopo sasa, tujue hakika hatuna kwa kukimbilia,” alisema.Mkoani Tanga, imamu wa Msikiti wa Ibadhi, Sheikh Mohammed Said aliitaka jamii kudumisha amani na utulivu uliopo na kuacha kushabikia vyama vya siasa.
Sheikh huyo alisema ni wajibu wa kila mtu kutambua kuwa amani iliyopo ikitoweka ni vigumu kuirejesha na hivyo kila mmoja ahakikishe anatambua wajibu wake.
Alisema wakati wa uchaguzi, hutokea jamii kuhamasishana kwa mambo ya kisiasa, jambo ambalo alisema ni baya na halifai kutokea na hivyo kutaka kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake.Mkoani Lindi, Sheikh Salimu Nalinga akitoa salamu za Eid el Fitr aliwataka Waislamu kuchagua viongozi waadilifu ili kuifanya nchi kuendelea kuwa ya amani na utulivu.
No comments