Ufafanuzi Wa Tanesco Kuhusu Tozo Ukinunua Umeme Kupitia Simu
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limezungumzia tozo ya asilimia 1.1 wanayokatwa wateja baada ya kununua umeme kwa njia ya mitandao ya simu na kupitia kwa mawakala wa benki.
Utaratibu huo ulianza Aprili 2 baada ya mfumo wa malipo wa Tanesco kuunganishwa na ule wa Serikali (GePG) ambao utawalazimu wateja wa huduma hiyo kulipia gharama za miamala husika, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo huduma hiyo ilikuwa ikitolewa bure.
Akizungumza jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema kuwa bei ya umeme bado haijapanda iko palepale kama ilivyokuwa awali.
“Hizi taarifa za kupanda kwa gharama za umeme siyo za kweli, hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu bei ilipitishwa na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji), hivyo hatuwezi kupandisha bila wao kuridhia,” alisema Dk Mwinuka.
Alisema tozo baada ya kununua umeme si kitu cha ajabu kwani watu wa mitandao hawawezi kumfanyia mtu huduma bila kuigharamia.
Meneja Masoko wa Tanesco, Mussa Chowo alisema utaratibu uliopo siyo mpya kwa kuwa kulikuwa na mkataba baina ya Serikali na mitandao ya simu kuwa na tozo kwa anayenunua kwa njia ya simu.
Alisema sehemu ambayo mteja atanunua umeme bila tozo ni ofisi za Tanesco, Benki ya NMB na CRDB, lakini kama watanunua kwa wakala wa benki watatozwa asilimia 1.1.
Alisema mteja akinunua umeme wa Sh5,000 atachajiwa Sh55 na atakayenunua umeme wa Sh10,000 atatozwa Sh110 na umeme wa Sh100,000 atatozwa Sh1,100.
No comments